Abstract
Ngano ni sanaa ya usimulizi ya Kiewe ambapo usimulizi, utendaji na ubunifu zinaungana pamoja katika mfumo wa kifasihi na mtu mmoja au kundi la watu. Tunasema mtu mmoja kwa maana ya kuwa baadhi ya mbinu zinazotumika zinategemea uwezo wa kifasihi wa msimulizi. Vilevile, zinaweza kuwa kwa kundi la wasimulizi kwa sababu baadhi ya mbinu zinazotumika ni kutoka katika jamii na zinagunduliwa pamoja na jamii. Utanzu wa ngano (ambao kwa Kiewe ni Gli) huchukuliwa na Waewe kuwa ni usimulizi wa mdomo unaotumia mbinu za kifasihi za kuwakilisha tamaduni na maisha ya jamii hiyo. Kumbo hii ya fasihi simulizi inatumika kuelimisha jamii ambayo inakuwa katika mfumo wa kuchanganya maadili, mafunzo na burudani kwa pamoja. Maudhui muhimu katika Gli ni kukemea tabia mbaya, ambayo haikubaliki katika jamii, na kuhimiza tabia njema, zinazokubalika katika jamii inayohusika. Hali kadhalika, ngano hutumika kuwatia moyo wanajamii katika shida na matatizo mbalimbali. Ngano nyingi hutumia mbinu mbalimbali za kifani katika uwasilishaji wa maudhui yake. Miongoni mwa mbinu maarufu zinazotumiwa na ngano ni matumizi ya motifu, na hasa motifu ya safari ya msako. Motifu hii hutumiwa kuwahamasisha wanajamii kujitafutia maisha mazuri kupitia safari ya msako. Aidha, hutumika kuibua maadili mbalimbali muhimu kwa jamii hii. Katika makala haya, tunajaribu kuwasilisha namna ngano za Kiewe zinavyoonesha utofauti katika ruwaza ya shujaa kwa mujibu wa Campbel. Kwa kuzungumzia suala hili, makala haya yamezingatia masimulizi ya ngano za Kiewe yenye motifu ya safari ya msako.

This work is licensed under a Creative Commons Attribution 4.0 International License.
Copyright (c) 2025 Jarida la CHAUKIDU
